Advancing

Kesho

Tunaihofu kesho! Itakuwaje kesho? Itakuwa tupu ama itajaa hamu na fanaka? Kazi imesimama. Maisha yamekwama? Hamu ya chochote haipo tena. Unyamavu umechukua kila sehemu ya nafsi na kiwiliwili. Roho zinaumia. Miili nayo inaliwa na funza pasi na kujua kwa wenye hiyo miili. Uvundo. Machozi. Vitisho vya kukatiziwa maisha na kunyimwa haki za kibinadamu. Maana’ke moyo kuhofu kesho.

Lakini Mbona kimya basi? Ama ni kuogopa kufa? Wimbo mtamu umekwisha? Umebadilika na kuwa wimbo wa uchungu, tamaa na hofu? Lawama tu kila upande.

Vivuli. Vivuli vya magofu ya watu. Mfano wa watu. Walikuwa watu hapo nyuma. Awali kabla ya kuporomoka, walikuwa wa maana. Wenye umahiri na nguvu. Lakini sasa wamebaki tu vivuli vya magofu visivyo na maana. Hata mwangaza huwakimbia.

Jana imepita. Mpito mpya unakolea. Upweke tu ndio uliobaki. Pepo za hasira zinavuma. Kiu na njaa zimekita. Kufululiza tu kwa maono ingawa hamna nguvu za kujiendeleza.

Safari ‘mefika kikomo. Maguu dhaifu yamechoka kusimama. Ari tu ndiyo imebaki. Kambi tuipige. Tupalilie kile tulichonacho. Kesho itafika.

Standard
Advancing

Nyakati zinageuka

Alijikataza kuwaza kwa vyovyote vile kuhusu yale ambayo yanampita katika dunia yake ya nje na ndani.Wakati mwingine alimchukia. Na pia aliweza kumheshimu na hata kumpenda mara nyingine. Ndoto tu. Lakini ndoto pia ina mwisho wake. Kujidanganya na kudanganywa. Iweje lakini kuingia bila ya kufikiria katika mtego huu? Amedanganywa. Lakini nani kamdanganya? Mbona basi aliyakubali yale alo’ahidiwa? Au ni ujinga tu? Labda ni kudharauliwa kiasi cha kutulizwa kwa hadaa ya maneno yasio na mbele wala nyuma.

Anaishi. Vyovyote viwe! Ingawa nguvu hana na urembo unamtoroka. Mizigo imekuwa nyingi. Hana hakika atajikwamua vipi. Kwa nini dunia imebadilika namna hii, hadi kukosa mlo ni kawaida? Mbona mshahara wako hauwezi kukuweka zaidi ya juma moja? Kwa nini bei za vitu zinakimbia kwa kasi na kutuacha chini tusizimudu?

Aaaa! Kwa nini lakini mwanadamu amekataa kuachana na zamani? Kuporomoka uliporomoka. Huwezi tena kuishi kama jana. Mbona kukabiliana na zamani ilhali uko karibu na kesho? Jana haikutiki! Huwezi kufanikiwa kwa kuishi maisha ya mwingine.

Standard
Advancing

Mpende akupende

Msisimko wa kimaisha haujamfadhaisha. Yu’ makini ili kuendeleza anachodhania muhimu kwake. Amepitia mengi. Ameona mengi. Amejitia hamu. Amefaulu kwa kiasi fulani.Rotuba ameitilia. Mbegu kuzipanda na kuupalilia huu alo’jiwekea.

Mapenzi kwake ndio kina cha maisha. Amempenda huyu bwana tangu amuone kwa mara ya kwanza. Amejizatiti kukubali na kumchukua jinsi alivyo. Amejaribu kila awezalo ili kumfurahisha. Kama ni mapenzi amempa. Chakula anampakulia na hata kumlisha wakati mwingine iwapo hajiwezi. Mtoto wa kike amempa. Tena mrembo sana. Kazi zote na mahitaji yake anatekeleza.

Mume lakini hana ahsante. Kila uchao ni vita. Vita vya maneno. Matusi. Kelele. Kujifanya eti hili au lile halijafanywa vile itakikanavyo. Kazi kukaa tu na kungojea apewe. Hata kama wote wamefika kutoka kazini. Yeye hujiona amechoka. Mkewe yuamdhania hana uchovu. Hana huruma huyu! Pengine ni hali ya kuwepo.

Mapenzi. Mapenzi. Kupenda. Kupendwa. Kudekezwa. Ndio maana yake nini? Iwapo kuna anayependa na hapendwi, kuna haja kweli? Mpende akupendaye na muhasi aso’kupenda. Hii ni muhimu kama unajipenda! Aaah. Fikra za nafsi iliyopotea!

Standard
Advancing

Tamu ya maisha

Kukosa au kumiliki jambo moja. Maisha au uhai wa mwanadamu yeyote ni kubahatisha tu. Hakuna anaye hakika ya wakati atakapo kata roho. Kuzaliwa ni kwa bahati, kuishi ni kwa Majaaliwa, lakini kifo ni lazima.

Tamu ya kuishi lakini ndio ipi? Ni kuwa na hela au mali kwa wingi? Au ni kuwa na jamii kubwa yenye upendo kila upande? Au ni marafiki wanao kupa raha kila uchao? Ama ni ule mhemko unaompata mtu akijilamba midomo baada ya chakula kitamu? Ama pia ni ule umahiri utokanao na ukubwa au kujulikana kisiasa?

Japo yote hayo yana umuhimu fulani kwa watu wengine, kunao wale walo’ na mtazamo tofauti. Kwao utamu wa maisha ni kuishi bila ya vurugu yoyote kila siku. Wengi wao hudhania eti kumcha na kumti Mola ndio hasa itampa mtu raha ya kuishi. Eti baadaye akhera watatunukiwa na maisha yaso’ kikomo.

Labda kuna ukweli kila upande. Au labda yote ni ndoto tu na hakuna chochote kiitwacho tamu. Ni fikra tu za kibinadamu za kujaribu kujiweka bila ya bugudha za hapa duniani.

Standard
Advancing

Majaaliwa

Lawama. Machungu. Hasira. Fedheha. Njaa. Hitaji za kila aina. Uhai tu ndio hakikisho kwa sasa. Lakini hakikisho ni lipi? Nani alo’ na uwezo wa kuumenya ukweli na kuyazalisha matunda ya uhuru? Labda uhuru tulo’ambiwa ni hekaya tu! Hamna hamu wala jitihada kwa vyovyote vile kuendeleza jamii. Haja tu ni kujitajirisha na kutumia binadamu wengine kama mtaji au malighafi.

Aaah. Lakini lawama, machungu, hasira, fedheha na njaa ya nini? Kimbelembele tu! Ama ni hali ya kuzikosa fedha? Au ni mapuuza ya kibinadamu? Zamani ubinadamu ulitawala na utu kutanda. Usasa ukaja na kumwacha kila mja ajitegemee. Hata kama utamrusha mwenzio ili upate utakacho. Muhimu ni kujilisha na kumpuuzilia mwenzio.

Sikio la akili. Bumbuazi kuondoka na fahamu kurejea. Macho yenye machozi na wekundu. Mtazamo wa dhamira fulani. Labda kila kitu huishia nguvu mbali na mwanzo wake. Hatima ya kila mja ni kifo.

Harufu tamu baada ya kula kila kitu na kubakia ombaomba. Labda ni ishara ya mafanikio ahera. Ama tu ni mwisho wa vita baina ya nafsi ya ndani na nje.

Standard
Advancing

Resi ya kumbukizi

Kuna raha katika ujana. Raha ya kufukuza unachokitaka, kupata usipate potelea mbali! Raha ya kutaka ushindi. Ya kuhisi una nguvu na kwa sababu hiyo unaweza kufanya chochote, na ukifanya lazima ushinde. Lazima ukitie mikononi unachokitaka.

Mpito.

Zamani kulikuwa na kile kilichoitwa neema. Ikiwepo  neema imani nayo hutawala. Neema ni sabuni na maji kwa roho zetu wanadamu.

Afrika ni maskini na hatujafanya maendeleo ya maana kwa sababu wamenyonywa kwa muda mrefu na wanaendelea kunyonywa. Na kwa bahati mbaya baadhi yetu tunaendelea kuupalilia unyonyaji huo kwa maslahi yetu.

Standard