Advancing

Jogoo Jata

Mparapata wake ndio tu uliomkashifu na kumfanya akosewe heshima na wale waliomdharau na kumuona eti yeye ni mtu aso’ maana. Wanaume wenzake ndiyo waliomchukia. Walimdhihaki na hata kumlaani. Vya dunia hakuwa navyo. Aling’ang’ania maisha kila siku kama waja wenzake pale kijijini. Alijaribu kila awezalo ili kujikweya katika hali na mali lakini hakufanikiwa bado. Umaskini ulimuandama toka jadi ya utotoni mwake. Inasemekana kuwa jamii yake tangu hapo zama za mababu ilikuwa ya kubahatisha tu na hawakuwa wa maana sana. Pesa siku hizi zimeadimika na wachache tu ndio walo’ nazo.

Ingawa haya yote yangemfanya mtu yeyote afedheheke, kwake Jata yalikuwa tu mambo ya kumpunguzia ushupavu wake. Yeye Jata ni mtu wa watu. Ndiyo. Mtu wa watu na hasa vichuna wote pale kijijini na vijiji jirani. Jina lake lilinawiri katika jamii ya wanawake, hata wale waliokuwa wameolewa walimsifu. Alikuwa Jogoo mkubwa katika makoo ya kuku!

Alipofikia umri wa kutanabahi maswala ya uhusiano wa nke na ume, Jata alibaini kuwa yeye ni shujaa. Alitumia hali hii kujikwamua na kujaribu kupunguza mori aliokuwa nao kutokana na umaskini wake. Alitaka kufurahisha nafsi yake. Aliwatumikia wote wa jinsia ya nke bila ya kujali walikuwa wa jamii ya mkubwa au wa maskini wenzake. Wanaume wa kijijini chao na jirani walimchukia kwani yeye tu ndiye aliyetambuliwa kama janadume wa nyakati zile.

Walipochoka na unyang’anyi wa wake zao, wanaume wa kijiji chao walipanga njama dhidi ya Jata. Walimwibia mparapata wake na kuuchoma moto. Kisha walimuandama usiku mmoja na kumpiga hadi akafariki dunia. Wanawake waliomwabudu Jata walishikwa na mori na kuwagomea waume wote. Waliamua kutoshiriki uhusiano na wanaume wa kijiji chao. Hii iliwalazimu hao waume waende mbali kutafuta kuchumbiana. Wale waliokosa hali na mali ya kwenda mbali, walibaki mle kijijini na kuolewa na tembo. Siku hizi ni walevi chakari waso’ mbele wala nyuma. Wamebakia kama mabofu yaliyotobolewa na kutolewa hewa!

Standard
Advancing

Hisia tu….

Ha! Hivyo ndivyo dunia ilivyo. Maisha. Au tuseme kung’ang’ania tu uchache uliopo na kudhania tunayo maisha. Wachache wanaishi. Wengi, kama sio wote, hawana maisha. Kuamka kila uchao wakiwa na hamu ya maisha. Lakini ng’o! Hiyo ni ndoto tu! Wale wanaoketi na kushikilia sehemu muhimu uongozini hawezi kuruhusu hata kwa chembe ya mchanga kuwaona watawaliwa wanaishi maisha afueni. Wakiwa na maisha, nani atakaye hadaiwa na kuwachagua uongozini?

Haki. Haki ya maisha na ya kila anachohitaji mtu ili kuweza kuishi haipo tena. Lakini haki ndio nini hasa? Labda ni mawazo tu ya wale was’okuwa na nguvu ya kufanya na kupata watakayo. Mfano ni wale wenye nyadhifa serikalini. Kwa muda wote huwa wanawakanyagia wapinzani wao kila upande. Lakini ikigeuka na wao ndio wako katika upinzani, hulalamika eti wananyanyaswa na kunyimwa haki zao na wale wal’o serikalini. Ah! Makubwa hayo! Tuyasaze kwa sasa kwani mawazo na fikra hayamlishi binadamu.

Usanii na ushairi haufi. Utabakia papo hapo miaka na mikaka. Lakini kwa nini binadamu huishi muda mfupi tu? Kwa nini hufa? Kwa nini hana aushi ya sanaa na ushairi? Labda ni njaa tu! Njaa ya matamanio na unyanganyi kila upande. Lakini nani asiyefikwa na msiba hapa? Mara huyu kafanyiwa hili au lile, huyu hana chakula, huyu ana kiu, ama huyu kalemewa na ugonjwa ilhali hana matibabu wala dawa.

Kutafuta maisha na uhali ni kitu cha maana sana. Kila afanyalo binadamu ni katika hiyo harakati ya kutafauta maisha. Hali tetezi lakini hutokea kila mara mtu atakapo kitu fulani. Au tuseme sio tetezi bali ni kitendawili tu. Shutuma upande mmoja na msaada upande mwingine. Mkinzano wa aina yake!

Standard